Polisi: Mwanafunzi aliyetoweka ‘alijiteka’
Jeshi la Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na polisi mkoani Iringa limebaini na
kujiridhisha kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul
Nondo hakutekwa, bali ‘alijiteka’ mwenyewe
Akizungumza leo
Jumanne Machi 13, 2018 kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema polisi
watachukua hatua za kisheria kwa kuwa mwanafunzi huyo amewadanganya watu
kuwa ametekwa na kusababisha taharuki kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Mambosasa amesema
polisi wamefanya uchunguzi na kubaini mwanafunzi huyo hakutekwa bali
‘alijiteka’ mwenyewe ili kutafuta umaarufu wa kisiasa na kusababisha kuzua
tafrani kwa jamii.
Amesema Machi 6, 2018
saa sita usiku zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Nondo
ametekwa na watu wasiojulikana.
Amebainisha kuwa
polisi wa kdana hiyo walianza kufuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo ikiwa
pamoja na kufunguliwa jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba
DSM/KIN/CID/P.E/51/2018.
Mambosasa amesema
Machi 7, 2018 walipewa taarifa na polisi mkoani Iringa kuwa mwanafunzi huyo
ameonekana Wilaya ya Mafinga akiwa na afya njema na mwenye kujitambua
akiendelea na shughuli zake.
“Mwanafunzi huyu
alionekana Mafinga akiendelea na shughuli zake na wala hakuripoti tukio la
kutekwa katika kituo chochote cha polisi hivyo tunaendelea kumshilikia hivyo
taratibu ili tumpeleke mahakamani,”amesema Mambosasa.
Amesema upelelezi
umebaini mwanafunzi huyo alikwenda kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akifanya naye
mawasiliano mara kwa mara akiwa njiani kuelekea Iringa.
Mambosasa amesema
kuwa pia alivyopimwa alionekana mwenye afya njema, hakupewa dawa yoyote ya
kumlevya na hakuwa na majeraha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni