Dstv Tanzania

CHUO KIKUU CHA KILIMO SOKOINE MOROGORO(SUA) WAMEKABIDHIWA MAJENGO KWA AJILI YA KUANZA KAMPASI MPYA YA TUNDURU MKOANI RUVUMA MSIMU MPYA WA MASOMO 2018/2019

 * Wananchi kijiji cha Daraja mbili waridhia kutoa ardhi zaidi ya Hekari 500 kwa ajili ya upanuzi wa Chuo.

* Wanafunzi wanaotaka kujiunga na Mwaka mpya wa masomo 2018/2019 wanakaribishwa kujiunga na kozi kwa ngazi ya cheti na stashahada kwa kuanza Tour Guide, Information Technology(IT), Utunzaji wa Kumbukumbu(Record Management) na baadae kozi za kilimo, mifugo, wanyama pori, misitu, ufugaji na maswala ya utafiti.

* Trekta moja kati ya 10 yaliyotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli litaletwa Tunduru kwa ajili ya maandalizi ya Shamba darasa kwa wanachuo na wananchi kwa ujumla.


WANANCHI wa Kijiji cha Daraja mbili katika kata ya Namwinyu Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma  wameahidi kutoa Ardhi Bure kwa ajili ya matumizi ya Chuo cha kilimo (SUA) ikiwa ni kivutio kwa chuo hicho kuharakisha ukamilishaji wa shughuli zake.

Ahadi hiyo ilitolewa na Wananchi hao katika hafla fupi ya makabidhiano ya majengo yaliyo kuwa kambi ya Wakandarasi wa shauri wa kampuni iliyojenga barabara kwa Kiwango cha lami Kilimesera-Matemanga. 


Wananchi ambao walitoa tamko hilo kwa pamoja katika mkutano huo wakiwa wanajibu kauli mbali mbali za viongozi walisema kuwa mbali na Mkutano mkuu wa kijiji hicho wapo tiyari kutoa zaidi ya hekari 500 kwa ajili ya matumizi ya chuo hicho lakini wapo tayari kuongeza endapo kutakuwa na mahitaji zaidi.

Kauli hiyo ambayo pia ilisisitizwa na Diwani wa Kata hiyo Mhe. Thabiti Said walisema kuwa ujio wa chuo hicho katika eneo la kijiji chao kutasaidia kupanua kujengeka kwa Kijiji, kuharakisha maendeleo  pamoja na kuwasaidia kuelimisha ndugu, jamaa na watoto wao hali itakayo wafanya kuanza kulima kilimo cha kisasa.

Awali Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda aliwaeleza wananchi hao kuwa katika utekelezaji huo, Chuo hicho ambacho endapo watakipokea kwa kupeleka wanafunzi wengi kila mwaka kitakua haraka na kuwa chuo kinacho jitegemea katika kipindi kifupi kijacho.

Prof. Chibunda aliendelea kubainisha kuwa katika utelekezaji huo chuo kimejipanga kuanza Oktoba mwaka huu kwa kutoa mafunzo katika Nyanja za utalii, Teknolojia na Utunza kumbukumbu ila baadae kitajitanua na kuongeza Kilimo utaalamu wa Vipando, Ugani, lishe,Tiba za wanyama, uzalishaji wa Lishe ya Wanyama, Ufugaji wa samaki, sayansi ya utunzaji wa mazingira, misitu na wanyama pori, kilimo Biashara pamoja na mafunzo ya maendeleo ya vijiji.

Alisema katika kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinaanza haraka na kuleta tija kwa wananchi wa maeneo hayo Chuo hicho kimepanga kupeleka Trekta moja kati ya marekta 10 waliyokabidhiwa na Mhe.  Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni na kuanzisha mashamba darasa ambayo yatasaidia wananchi wengi kwenda kujifunza kwa vitendo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mhe. Mkwanda Sudi alisema kuwa katika utekelezaji huo kwa kuanzia Wananchi hao wamekubaliana kutoa Hekta 9 na Majengo 11 ambayo yalitumika na wakandarasi washauri wakati wa ujenzi wa barabara ya lami.

Mbunge wa jimbo la Tunduru kusini Mhe. Daimu Mpakate alisema kuwa ujio wa Chuo hicho ni ukombozi wa wananchi waishio Mikoa ya pembezoni ikiwemo Wilaya ya Tunduru pamoja na wilaya zilizopo katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera aliwataka wananchi kujipanga kwakupeleka Watoto wao Shule na kuhakikisha wanafaulu vizuri ili chuo hicho kiweza kuwanufaisha wakazi wa Tunduru, Namtumbo na watanzania wote kwa ujumla.

Alisema kwa vile Chuo kipo Tunduru itapendeza endapo kutakuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaotoka ndani ya wilaya ya Tunduru na wengine maeneo ya jirani kama Namtumbo, Nanyumbu, Masasi na Tanzania kwa ujumla.

Hakuna maoni: