Benki Ya Standard Charted Kuimwagia Tanzania Sh. Trilioni 3.3 Kujenga Reli Ya Kisasa-SGR
BENKI
ya Standard Chartered Group imekubali kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa
dola za Marekani bilioni 1.46 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 3.3 kwa
ajili ya kujenga kipande cha Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR)
kuanzia Morogoro hadi Makutupora, mkoani Dodoma.
Hayo
yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, baada
ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo
Bw. Bill Winters, Jijini Dar es Salaam.
Dkt.
Mpango ameishukuru Benki hiyo kwa kukubali kugharamia ujenzi wa Reli
hiyo ya kisasa ambayo lengo lake ni kuimarisha usafiri na usafirishaji
wa abiria na mizigo kwenda bara na nchi jirani za Maziwa Makuu na zile
ambazo hazipakani na Bahari.
"Tunajenga
Reli hiyo ya Kisasa kutoka Dar es Salaam - Morogoro hadi Makutupora
ambazo ni awamu mbili lakini pia tutajenga reli hiyo kuelekea Isaka
mpaka Mwanza na baadaye Rusumo ambapo wenzetu wa nchi ya Rwanda,
tutasaidiana, wao watajenga reli hiyo kutoka Rusumo hadi Kigali"
Aliongeza Dkt. Mpango
Aidha,
Dkt. Mpango amemweleza Kiongozi huyo wa Juu kabisa wa Benki ya Standard
Chartered Group anayeongoza Benki hiyo kwenye nchi zaidi ya 60 duniani,
kuhusu vipaumbele vikubwa vya nchi ikiwemo kuboresha Shirika la Ndege
la Taifa-ATCL, na Ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme wa Mto Rufiji.
"Tunaimarisha
Shirika letu la Ndege ili kuimarisha sekta ya utalii kwa sababu tuna
vivutio vingi na haipendezi wageni wanao kuja nchini wanafikia nchi
jirani, sasa ifike wakati tuwe na uwezo wa kuwasafirisha moja kwa moja
kuja nchini kwetu" Alisisitiza Dkt. Mpango.
Alisema
Tanzania ni ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii
ikitanguliwa na Brazil lakini inapokea watalii wasiozidi milioni 2 kwa
mwaka jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka ili sekta hiyo
ichangie uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa kupitia fedha za kigeni.
Alisema
katika kulifufua Shirika hilo la Ndege, tayari Serikali imenunua ndege
nne ikiwemo ndege kubwa aina ya Boeing 787- 8 Dreamliner na kwamba ndege
nyingine 3 zitakuwa zimewasili nchini ifikapo mwezi Juni, mwakani, na
kulifanya shirika hilo kuwa na ndege 7.
Alivitaja
vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha huduma za jamii kama vile elimu,
afya, maji na kuendeleza ujuzi kwa wananchi ili waweze kufanyakazi
kwenye viwanda na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa ujumla kwa kuwa
maendeleo yanahusu watu.
Akizungumza
kwenye mkutano wake na Dkt. Mpango, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Standard Chartered Group, Bw. Bill Winters, ameipongeza Tanzania kwa
kupiga hatua kubwa kiuchumi na kwamba Benki yake itatoa mkopo huo na
kuahidi kuwa balozi wa kuelezea mafanikio makubwa ya kiuchumi ya
Tanzania kwa wadau wengine.
Aliahidi
kuzishawishi taasisi nyingine za fedha ulimwenguni kuangalia uwezekano
wa kuunga mkono jitihada hizo ambazo mwisho wake wanufaika wakubwa
watakuwa ni wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla.
"Tunaimani
kubwa na uwezo wa Tanzania pamoja na fursa nyingi za kiuchumi ilizonazo
na kwamba miradi mingi ya kipaumbele iliyoainishwa itafikiwa na tunalo
jukumu kama Benki kutoa fedha na kuiweka miradi hiyo pia sokoni ili
iweze kupata fedha" Alisisitiza Bw. Bill Winters.
Katika
kikao hicho, Bw. Bill Winters aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki hiyo nchini Kenya na nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Lamin
Manjang na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo nchini Tanzania Bw. Sanjay
Rughani, ambapo pia Benki hiyo inafanya shughuli zake hapa nchini kwa
kipindi cha miaka 101 sasa.
Mwisho
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni