MANGULA ATOA NENO WANACCM KUMKATAA ALIYEITOSA CHADEMA
Siku moja baada ya
kundi la wanachama wa CCM kujitokeza hadharani kupinga aliyekuwa mbunge wa
Monduli, Julius Kalanga kurejeshwa kugombea ubunge kupitia chama hicho, Makamu
Mwenyekiti wa CCM - Bara, Phillip Mangula amesema hiyo ni hofu tu lakini hakuna
mpango huo.
Akizungumza na wanahabari
Mangula amesema Kamati Kuu ya chama
hicho itakaa mwezi ujao kuamua nani asimamishwe kwenye uchaguzi wa Monduli na
majimbo mengine ikiwa ni baada ya kupata maoni ya chama kuanzia ngazi ya jimbo,
mkoa na halmashauri kuu.
Kuhusu waliohama
vyama vyao na kusimamishwa tena kugombea kwenye majimbo yaleyale, Mangula
alisema wao wenyewe (jimboni) walitaka iwe hivyo ndiyo maana wagombea hao
wakapewa nafasi.
“Wahusika walitaka
iwe hivyo ndiyo maana wakapewa nafasi. Kwa mfano jimbo la Kinondoni,
aliyepitishwa na chama alipata kura zaidi ya yule aliyegombea kwenye uchaguzi
mkuu uliopita,” alisema kiongozi huyo wa chama.
Juzi, baadhi ya
wanachama wa CCM kutoka kata za Isilalei, Monduli Juu na Sepeko waliandamana
hadi ofisi za chama wakimtuhumu Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Wilson
Lengima kwamba kwa kushirikiana na viongozi wengine wa chama hicho, wanapanga
njama ili Kalanga apitishwe kuwa mgombea ubunge pasipo kufanyika kwa kura za
maoni.
Hata hivyo, Lengima
alikanusha madai hayo akisema CCM ina utaratibu wake wa kuwapata wagombea wa
nafasi mbalimbali za uongozi, hivyo kuwataka wanachama wa CCM kuwa watulivu.
Katibu wa Uenezi wa
CCM Kata ya Sepeko, Nooy Naimisye alisema jana kuwa wanataka kuona demokrasia
ikitendeka katika kumchagua mgombea ubunge jimboni Monduli.
“Mwenyekiti atupe
ukweli kuhusu madai kwamba yupo upande wa mbunge wa zamani aliyejiuzulu Chadema
na kutangaza kujiunga na CCM. Tunataka demokrasia hatuna nia kuona mgombea huyu
anagombea tena kwenye chama chetu, hili ni kinyume cha kanuni na utaratibu
ndani ya chama,” alisema.
Wakati hayo
yakiendelea, mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ameandika kwenye ukurasa wake wa
Twitter:
“Chama hiki kina
katiba, sheria, kanuni na utaratibu/utamaduni, ni vizuri wahamiaji wakasaidiwa
kuvifuata ili kulinda umoja na mshikamano wetu.”
Alipotafutwa
kufafanua maana ya maneno hayo, Nape hakupokea simu wala kujibu ujumbe wa
maneno aliotumiwa.
Hata hivyo, baadhi ya
wananchi wameandika kwenye ukurasa wa mbunge huyo. Elibariki Magesa amesema:
“Haya maneno Waitara na Kalanga hawataki kuyasikia kabisa wanatamani kurudi
walikotoka lakini haiwezekani. Bila huruma za mwenyekiti hawa ndugu zetu
wazalendo watapata vichaaa, ‘assume’ kura za maoni wapingwe na pensheni wakose
si wazalendo ‘let it be’ (na iwe hivyo).”
Sylvester Muyigwe
ameandika: “Kama kuna mahali Katiba ya nchi imekanyagwa na wewe na wenzako
mkashangilia mkiona kuwa wamekomolewa Chadema au yoyote asiye wahusu basi
eleweni hata hiyo ya chama itakanyagwa zaidi ya hii ya nchi na hamtakua na
lakufanya.”
Meyasi Mollel
ameandika: “Tuna tatizo kubwa sana katika siasa za nchi yetu na wanasiasa
wanatupeleka pabaya sana. Siasa safi ina katiba, sheria, kanuni na utaratibu.
Bro, double standard ni hatari sana...”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni