MH. GULAMALI ATEMBELEA CHUO CHA TAIFA CHA USAFIRISHAJI (NIT) KUJIONEA MAPINDUZI MAKUBWA KATIKA SEKTA YA USAFIRISHAJI.
Na Francis Daudi,
Mbunge wa Jimbo la Manonga, Mweshimiwa Seif Khamis Gulamali amekitembelea Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT ambacho kimejidhatiti kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya Usafirishaji nchini Tanzania kwa kuzalisha wataalamu Zaidi.
Chuo Hicho ambacho kilianzishwa Mwaka 1975 ni katika Vyuo Vya Mwanzo kabisa kuanzishwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwl.Julius Nyererere kwa lengo la kuhakikisha Inakuza Sekta ya Usafirishaji Nchini.
Akiwa Chuoni hapo Mh. Gulamali ambaye amewahi kusoma katika Chuo hicho miaka 8 iliyopita na pia kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi alipokelewa na Mkuu wa chuo Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa.
Mkuu wa chuo hicho ameeleza mipango ya Chuo hicho na hatua walizofikia ili kuhakikisha kinakuwa Chuo Kikuu cha Usafirishaji nchini Tanzania na Afrika nzima. Chuo cha NIT kimepata fedha karibu Shilingi Bilioni 140 toka Serikali ya China ili kujenga majengo na kuimarisha miundo mbinu katika chuo hicho na Kuwa Chuo Kikuu cha Usafirishaji.
Profesa Mganilwa ameeleza Chuo hicho kinatia juhudi pia katika kuzalisha wataalamu bora kabisa ili kwenda na kasi ya Serikali katika kujenga miundo bora ya Usafiri nchini Tanzania. Pamoja na mambo mengine chuo kimeanzisha kozi zinazoendana na uhitaji wa soko la ajira kama vile Bachelor of Aircraft Maintainance( Shahaha ya Marekebisho ya Ndege) na Bachelor of Education in Mathematics and Information Technology( Shahada ya Elimu katika Hisabati na Teknolojia ya Mawasiliano).
Fani hizi ni sehemu ya Fani nyingi zilizopo Chuoni hapo ambazo hazipatikani katika Chuo chochote hapa nchini. Ameongeza kuwa pia wamepeleka Wataalamu katika Nchi mbalimbali kama China, Korea na Japan ili kuongeza Ujuzi katika Uzamili na Uzamivu ili kuimarisha idara mbalimbali ndani ya Chuo cha NIT.
Chuo cha NIT kimepokea takribani milioni 400 toka Benki ya Dunia na Mashirika ya ndege duniani ili kusaidia kuzalisha Zaidi wataalamu bora katika sekta ya Usafirishaji hasa wa Usafiri wa Anga. Chuo cha NIT kinatarajia kupokea wataalamu toka Shirika la Boeing watakaofika kutoa mafunzo kwa wataalamu na wafanyakazi wa shirika la Ndege ATCL. Hii ni kwa kuwa chuo chicho ndio pekee chenye miundo mbinu na vifaa bora vya kufundishia masuala mbalimbali katika usafiri wa Anga.
Mh. Gulamali alipata fursa kutembelea Shule ya Usafiri wa Anga(School of Aviation) yenye Madarasa ya waendesha ndege, Karakana maalumu za kutengenezea Injini za Ndege na baadaye Idara ya ukaguzi wa Magari akiongozwa na Mkuu wa Chuo Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa. Katika kuhitimisha ziara yake katika Chuo hicho, Mh. Gulamali ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali pindi itakapohitajika.
Aidha, amesema kwamba chuo cha NIT kikiweza kutumika vizuri kitazalisha wataalamu ambao ni bora ili kwenda katika uchumi wa kati unaohitaji sekta madhubuti ya Usafirishaji wa bidhaa na watu.
Mwisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni