Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Serikali nchini China
Mkutano
wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na
China (FOCAC) utafanyika Beijing kuanzia tarehe 01 hadi 04 Septemba,
2018.
Ujumbe
wa Tanzania kwenye mkutano huo utaongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Viongozi
wengine watakaoshiriki Mkutano huo ni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga; Mhe.
Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na Mhe. Rashid Ali Juma, Waziri wa Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Viongozi wengine
Waandamizi.
Mkutano
huo utafunguliwa na Rais wa China, Mhe. Xi Jinping ambaye pia ni
Mwenyekiti wa jukwaa hilo, kwa kushirikiana na Mwenyekiti Mwenza, Rais
wa Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa, utahudhuriwa pia na
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Rwanda, Mhe. Paul
Kagame, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Antonio Guterres na
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika ambaye pia ni Rais wa Chad, Mhe.
Moussa Faki Mahamat. Mkutano huo pia utashuhudia uchaguzi wa Mwenyekiti
Mwenza mpya kutoka Afrika.
Kaulimbiu
ya Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika kwa mwaka
2018 ni “China na Afrika: Kuelekea Jumuiya Imara kwa mustakabali wa wote
kupitia ushirikiano kwa manufaa ya wote” (China and Africa: Toward an
Even Stronger Community with a Shared Future through Win-Win
Co-operation).
Mkutano
wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu
kitakachofanyika tarehe 01 Septemba, 2018. Kikao hicho pamoja na mambo
mengine kitapitia agenda za mkutano huo na kuziwasilisha kwenye kikao
cha Mawaziri kitakachofanyika tarehe 02 Septemba, 2018.
Mkutano
wa Jukwaa la Ushirikiano kati Afrika na China pamoja na mambo mengine
utajadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na China na
kufanya mapitio ya mikakati ya pamoja ya maendeleo iliyopo kati ya
Afrika na China.
Jukwaa
hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2000 huwaleta pamoja viongozi wa Afrika
na China kujadili masuala ya ushirikiano na maendeleo na kutathmini
utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa kati yao.
Aidha,
masuala ya ushirikiano katika uendelezaji Miundombinu kama Barabara,
Reli, Bandari na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Bara la Afrika
yatajadiliwa kwa kina.
Agenda
nyingine itahusu kilimo cha kisasa ambapo China itatoa uzoefu wake
katika kutumia sayansi na ubunifu wa kiteknolojia katika kufikia
uzalishaji wenye tija na kuongeza thamani kwa mazao ili kuwa na soko la
uhakika.
FOCAC
2018 pia itajadili masuala ya biashara na uwekezaji ambapo kwa kuona
umuhimu huo, Mhe. Xi Jinping, Rais wa China atafungua rasmi Mkutano wa
Jukwaa la Biashara kati ya China na Afrika utakaofanyika tarehe 03
Septemba, 2018.
Mkutano
wa kwanza wa Wakuu wa Nchi wa Jukwaa hili ulifanyika Beijing mwaka 2006
na Mkutano wa Pili ulifanyika nchini nchini Afrika Kusini mwaka 2015.
Wakati
wa Mkutano wa pili, China ilitangaza mpango kabambe wa kuhamasisha
mapinduzi ya viwanda na kilimo cha kisasa kwa Afrika wenye gharama ya
Dola za Marekani bilioni 60 katika utekelezaji wake.
Kufuatia
ushirikiano kupitia Jukwaa hilo biashara kati ya China na Afrika
imeongezeka pamoja na ongezeko la ushirikiano wa kiutamaduni na biashara
baina ya watu wa China na Afrika.
Pembezoni
mwa Mkutano huo, Tanzania na China zimeandaa Kongamano la Biashara
ambalo litafunguliwa rasmi na Mhe. Waziri Mkuu tarehe 02 Septemba, 2018.
Kongamano hilo ambalo litajadili kwa kina masuala ya uwekezaji na
biashara kati ya Tanzania na China litashirikisha takribani makampuni 80
kutoka nchi hizi mbili.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
30 Agosti 2018
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni