Dstv Tanzania

Mizengo Pinda Asema Wapinzani Watapata Tabu sana Wasipojitafakari Upya

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mizengo Pinda ametoa ushauri kwa vyama vya upinzani vijitafakari kwa nini viongozi wao wanawakimbia, vinginevyo watapata taabu sana.

Pinda ametoa ushauri huo aliouita ni wa bure kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kivule Kata ya Kivule, alipozindua kampeni za Uchaguzi Mdogo wa ubunge Jimbo la Ukonga wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam.

Alikuwa akimnadi mgombea wa CCM, Mwita Waitara ambaye alikuwa Mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kabla hajakihama na kurudi CCM hivi karibuni.

“Ajenda yao kuu upinzani ni kunung’unika pekee, watapata tabu sana, sio ile wa wapigwe tu, hii ni watapata tabu sana, wakae chini wajitafakari huu ni ushauri wa bure,” amesema Pinda ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu.

Pinda amesema kama wapinzani wataendelea kutoa majibu mepesi katika maswali magumu, wataona linalokuja mbele.

Amemuombea kura Waitara awe Mbunge wa jimbo hilo, huku akimtaka apuuze hoja dhaifu zinazodai kuwa amenunuliwa.

Amesema CCM haikukosea kumteua Waitara, kugombea kupitia chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Septemba 16, mwaka huu.

“CCM haiendeshi mambo yake kiholela, mpeni kura Waitara kwani CCM ilifanya maamuzi ya busara kwa kuzingatia mazingira na kuamua kumrudisha,” amesema.

Aidha, aliwataka wananchi kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kazi yake nzuri ya kupaisha uchumi pamoja na kuendelea kutatua kero za wananchi kila kukicha.

Amewashauri kuwa karibu na mabalozi, ambao ndio watakaosaidia kuomba kura kwa wananchi na pia kuendelea kubaini changamoto za wananchi na kuzitafutia majibu.

Waitara amesema upinzani wana hoja dhaifu kuwa amesaliti wananchi wa Ukonga, wakati wanajua kuwa mambo ndani ya chama hicho yalikuwa hayaendi, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kufanya kazi vizuri ya kutatua kero za wananchi.

“Mliponipigia kura nilipata tabu sana, kulikuwa na kero nyingi, lakini mizigo ndani ya Chadema ilikuwa ni mingi wananchi wakiniletea kero zao lazima niongee na viongozi wa serikali ambao wanatoka CCM ili wanisaidie, lakini nikionekana tu na viongozi natakiwa kujieleza,” alisema Waitara.

Amesema ukiwa Chadema, hawataki mtu kusema ukweli hasa kwenye mambo mazuri ambayo yanafanywa na Serikali ya CCM, badala yake wanataka utukane CCM bungeni.

Waitara aliyewahi kuwa Katibu wa UVCCM Mkoa, alisema mpaka sasa katika jimbo hilo lenye kata 13, hakuna hata kata moja ambayo haina miradi inayoendelea kutekelezwa na alipongeza jitihada hizo za serikali.

Amewaomba wananchi wa kata hiyo ya Kivule, ambako aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule kumpa kura ili arudi bungeni kuwatumikia na kuwa mtatuzi wa kero zao, kwani sasa atakuwa karibu na serikali kuliko alikokuwa (Chadema).

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rodrick Mpogolo amesema chama hicho kinakubalika kwa kiwango kikubwa nchini kwa sasa, hivyo wananchi wa kata hiyo na jimbo hilo kiujumla wasipoteze nafasi yao kwa kumchagua mgombea wa chama kingine.

“Na niwaambie tu hii ni awamu ya sita ya Uchaguzi Mdogo toka Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, kati chaguzi zote hizo kila ikitokea uchaguzi tunashinda kwa kishindo nawashauri Ukonga msipoteze fursa hii mumchague Mwita Waitara,” amesema Mpogolo.

Mjumbe mwingine wa Kamati Kuu, Makongoro Nyerere amesema hoja ya upinzani kuhusu CCM kuwa na mafisadi na wala rushwa, sasa imepotea na kwamba sasa wala rushwa wakuu ni wao.

Hakuna maoni: