Serikali Kutekeleza Miradi Kwa Kushirikiana Na Sekta Binafsi Yenye Thamani Ya Mabilioni Ya Shilingi
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali
ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuanzisha na kutekeleza miradi
mikubwa ya maendeleo kwa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP)
ambapo miradi zaidi ya 11 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji
lengo likiwa ni kufanikisha azma ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Idara ya Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. John Mboya wakati akiwasilisha mada ya utekelezaji wa dhana ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo nchini kwenye semina iliyowashirikisha mawaziri, naibu mawaziri na baadhi ya watendaji wa serikali iliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Akiwasilisha
mada hiyo, Dkt. John Mboya amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa umakini
mkubwa katika uandaaji na utekelezaji wa dhana hiyo ya ubia Sekta ya
Umma na Binafsi kwa kuzingatia sheria, sera, miongozo, kanuni na
taratibu mbalimbali zilizopo.
Aidha
alizitaka taasisi na wadau wa utekelezaji kuwa tayari kujifunza kutoka
katika nchi zilizoendelea kupitia dhana hii ya ushirikikishwaji wa sekta
binafsi katika kuchochea ukuaji wa viwanda na uchumi wa nchi kwa
ujumla.
Dkt.
Mboya aliitaja baadhi ya miradi iliyoko katika hatua mbalimbali ya
utekelezwaji kwa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi kuwa ni mradi
wa mabasi yaendayo haraka (DART), Ujenzi wa Viwanda vya dawa, mradi wa
VETA utakaohusisha ujenzi wa vyuo 10 ambavyo vinatarajiwa kutoa ujuzi
mbalimbali kwa wanafunzi wapatao 90,000 ili kukidhi mahitaji ya
wataalamu watakao saidia kufanikisha uchumi wa viwanda.
“MIradi
Mingine ni Ujenzi wa Bandari ya Mwambani, barabara ya Dar es salaam
hadi Chalinze, Ujenzi wa Reli kwenye miradi ya Mchuchuma hadi Mbambabay
mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara, Ujenzi wa Reli kuanzia Tanga, Arusha
hadi Musoma, na mradi wa umeme wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Akijibu
swali la Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Josesph Kakunda, aliyetaka kujua kuhusu kuondolewa kwa sheria
ya utekelezwaji wa miradi kwa Ushirikishwaji wa Pamoja kati ya serikali
na sekta binafsi (Joint Venture) ambayo haikufanikiwa kama
ilivyokusudiwa hapo awali, Dkt. Mboya alisema kuwa sheria hiyo
haijaondolewa bali miradi hiyo itatekelezwa kupitia sheria ya Kampuni.
Akichangia
katika mjadala wa semina hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya, alisema ni vema wakati wa kuchagua
miradi wahusika wawe makini ili kuepuka kuanzisha miradi inayofanana na
ambayo inaweza kuwa chanzo cha kufa kwa miradi iliyotangulia.
“Ninashauri
kuwepo kwa fursa ya ushirikishwaji katika miradi midogo ambayo ina
manufaa kwa wananchi ikiwemo ya ujenzi wa nyumba za waalimu” Alisema
Mhandisi Manyanya
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alizitaka taasisi ambazo
zinatekeleza miradi kwa ubia na sekta binafsi zielezee umma wa
watanzania mafanikio yaliyopatikana ili kuhamasisha wadau wengine
kufuata nyayo hizo huku akitolea mfano Shirika la Maendeleo ya Petroli
nchini (TPDC) ambalo nalo liko katika utekelezaji wa dhana hiyo.
Mwenyekiti
wa semina hiyo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji,
alisema kuwa Serikali imepeleka Muswada Bungeni unaohusu PPP, ambao
ukipitishwa na Bunge linalotarajiwa kuanza Septemba 4, 2018, utekelezaji
wa ubia huo utakwenda kwa kasi zaidi ili kuiwezesha nchi kufikia
malengo yake ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya wananchi.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge ,
Kazi,Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama, akiahirisha mafunzo
hayo, aliwataka wadau wa semina hiyo kuendelea kukutana na kuelimishana
hadi hapo marekebisho ya sheria hiyo ya Ubia Sekta ya Umma na Binafsi
(PPP) yatakapofanyika.
“Utekelezwaji
wa dhana hii ya Ubia Sekta ya Umma na Binafsi ndio njia rahisi
itakayosaidia kukamilisha miradi mingi ambayo imeainishwa katika ilani
ya uchaguzi ya Chama Cha Mapainduzi (CCM) na kwenye Mpango wa Maendeleo
wa Taifa wa Miaka Mitano, bila ushirikiano huu na sekta binafsi hatuwezi
kufikia uchumi wa viwanda kwa kasi inayotakiwa’’ Alisema Waziri
Mhagama.
Semina
hiyo ya siku moja imeendeshwa na wataalamu wa masuala ya Ubia Sekta ya
Umma na Binafsi kutoka Benki ya Dunia, ambapo Jumapili, kamati tatu za
Bunge zitapatiwa elimu na kujengewa uwezo kuhusu dhana hiyo ya PPP.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni