KATIBU MKUU CCM ATOA ONYO KWA WATAKAO HUJUMU MALI ZA CHAMA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Dk.Bashiru Ally
amesema Chama hicho kinadhibiti mianya ya ubadhilifu wa rasilimali fedha
na mali zake ili kijitegemee kiuchumi.
Alisema endapo rasilimali hizo zitatumika vizuri na kuanzishwa kwa
miradi mingine mikubwa ya uzalishaji wa kipato katika ngazi mbali mbali
za chama na jumuiya kwa kuwanufaisha wanachama wote badala ya watu
wachache.
Kauli hiyo aliitoa jana katika mwendelezo wa ziara yake kisiwani Pemba
wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa
Mikoa Miwili katika ukumbi wa Fidel Castro uliopo, Mkoa wa Kusini Pemba.
Dk.Bashiru alieleza kuwa lengo la kusimamia dhana ya ukuaji wa uchumi
ndani ya chama kupitia vyanzo vyake vya mali na fedha ni kukiondosha
chama katika mazoea ya kutegemea ufadhili wa watu wenye fedha wanaokuwa
na malengo ya kujinufaisha wenyewe kisiasa.
Pia aliyataja malengo mengine kuwa ni uimarishaji wa maslahi ya
watumishi wa CCM na jumuiya zake kwani bado maslahi yao ni ya kiwango
cha chini ambayo hayaendani na hadhi ya taasisi yenyewe.
“ Kwa miaka mingi chama chetu kimeondoka katika misingi ya kujitegemea
na badala yake kujitokeza kwa watu wenye fedha kukichangia chama wakati
wa uchaguzi na mazoezi mengine ya kitaasisi, sasa katika mageuzi haya ya
kimuundo tuna dhamira ya chama chetu kukiondosha uko na tukaweza
kutumia mali zetu wenyewe kujiendesha kitaasisi.” Alifafanua Dk.Bashiru.
Alieleza kuwa malengo hayo yakifanikiwa utakuwa ni ushindi mkubwa kwa
wanachama wa CCM wote kwani tabia za rushwa na makundi ya kusaka nafasi
za uongozi kwa kutumia fedha yatakuwa yamedhibitiwa.
Aliwataka viongozi wote wa taasisi hiyo kuunga mkono malengo hayo kwa
kuhakikisha wanapunguza matumizi holela ya fedha na badala yake
waanzishe miradi itakayowasaidia kujiendesha ili kulinda heshima na
hadhi ya CCM mbele ya jamii.
Pamoja na hayo alizitaka jumuiya zote hasa ya umoja wa vijana (UVCCM)
kuhakikisha wanakuwa wabunifu kwa kutumia rasilimia walizonazo kwa
kuanzisha miradi mikubwa ya kilimo, uvuvi na viwanda vidogo vidogo ili
vijana wajiajiri wenyewe.
Katibu Mkuu huyo Dk.Bashiru aliweka wazi msimamo wa Chama Cha Mapinduzi
kuwa wale wote waliohusika na kutapeli na kujimilikisha mali za taasisi
hiyo kinyume na utaratibu wote watachukuliwa hatua za kisheria.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi alisema
wanachama wote wana haki ya kuunga mkono mambo mema yanayotekelezwa na
taasisi hiyo kwa nia ya kuongeza ufanisi.
Alisema wakati wa vyama vya ukombozi vya ASP na TANU viongozi wa wakati
huo walifanikiwa kupanga mambo ya maendeleo yaliyodumu kwa muda mrefu
kutokana na umoja na mshikamano waliokuwa nao hasa katika masuala ya
kuvijenga kimaendeleo vyama vyao.
Dk. Mabodi alieleza kuwa suala la uzalendo katika kusimamia maslahi ya
kitaifa ni jambo muhimu hasa kwa viongozi wanaoaminiwa na kupewa dhamana
za kuongoza jamii.
Akizungumzia ushindi wa CCM visiwani Zanzibar mwaka 2020 alisema mpaka
sasa Zanzibar hakuna upinzani bali kuna vikundi vidogo vidogo vya watu
wanaojivisha joho la upinzani wakati wao ni madalali wa kisiasa
waliofilisika kifikra.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema CCM itashinda kisayansi kutokana na
serikali zake kutekeleza mahitaji ya wananchi wa mijini na vijijini
kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni