Dstv Tanzania

WABUNGE WAMLILIA MONICA MAGUFULI, ODINGA AVUTIWA NA WABUNGE VIJANA



IDADI kubwa ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana walijitokeza kwenye Mazishi ya Dada wa Rais John Joseph Magufuli, Bi Monica Magufuli aliyefariki dunia asubuhi ya tarehe 19 Agosti, 2018 katika hospitali ya Bugando Jijini Mwanza alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Wabunge na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Marais wastaafu walianza kuingia Mkoani Geita kuanzia juzi tarehe 20 Agosti 2018 ili kuwahi mazishi hayo.

Katika ibada ya mazishi iliyoongozwa na Askofu mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwaichi, Wabunge waliwakilishwa na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba Mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki pamoja na wabunge wengine wakiongozwa na Mbunge wa Manonga Seif Gulamali,  Mbunge wa Bukoba vijijini Jason Rweikaza, Mbunge wa Namanyele Ally Kessy, Medard Kalemani Mbunge na Waziri wa Nishati na Mbunge wa Karagwe Innocent Bashungwa.

Aidha mazishi hayo yalihudhuriwa na kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ambaye alivutiwa na idadi kubwa ya wabunge vijana waliofika kumzika Monica Magufuli.

Akizungumza na mwandishi wetu Mbunge wa Jimbo la Manonga, Mheshimiwa Seif Gulamali alisema: "Mwenyezi Mungu anatufundisha kuthamini zawadi ya Uhai na kuitumia vizuri, maisha ya bi. Monica yametuachia funzo kubwa la Upendo na Kujali wengine" ameeleza  Gulamali

"Kama tulivyomsikia Mheshimiwa Rais akielezea jinsi dada yake  alivyojitoa kuja kumuhudumia mama yake Bi  Suzana Magufuli ambaye ni mzee. Huu ni upendo usio kifani ambao sisi tuliobaki inatupasa kuiga" Aliongeza.

Aidha Mbunge wa Namanyele Ally Kessy aliyehudhuria msiba huo amewaasa viongozi hasa wabunge kushirikiana zaidi wakat wa misiba bila kujali itikadi zao za vyama.

Msiba huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Marais wastaafu, Makamu wa Rais Waziri Mkuu, Wabunge na viongozi wengine wa dini na Serikali.

Mwili wa Monica Magufuli (Dada wa Rais Magufuli ) ulizikwa  hapo jana katika makaburi ya familia yaliyopo ndani ya makazi ya Rais katika Kijiji cha Mlimani, Kata ya Muungano Wilaya ya Chato mkoani Geita. Monica Magufuli ameacha Mume, Watoto tisa na wajukuu 25.

Mwisho.

Hakuna maoni: