Makamu wa Rais Kuzindua Jengo la Kitega Uchumi la Ghorofa 16 Jijini Arusha
Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwaongoza maelfu ya wananchi
wa Mkoa wa Arusha katika hafla ya uzinduzi wa jengo la kitega uchumi la
Jakaya Kikwete Ngorongoro Tower (JKNT).
Jengo
hilo la ghorofa 16, ambalo ni mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA), linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Makamu wa Rais, Septemba 16,
mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari wakati walipotembelewa na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa wa Arusha, kukagua jengo hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya
NCAA, Profesa Abiud Kaswamila, alisema Makamu wa Rais amethibitisha
kuhudhuria katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo.
Alisema
jengo hilo ni kati ya majengo ya kisasa zaidi kujengwa mkoani hapa na
litatumika maalum kama kituo kimoja cha kukuza na kurahisisha biashara
ya utalii nchini.
Maneja
wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo, Profesa Camillius Lekule, ambaye
ndiye aliyebuni mchoro wa jengo hilo, alisema kiasi cha fedha
zilizotumika hadi sasa ni Sh. bilioni 39.9 kati ya Sh. bilioni 45
zilizokadiriwa awali.
Alisema
matarajio ya NCAA baada ya kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa mradi
huo gharama za ujenzi zitarudi baada ya miaka 20.
Alisema
jengo hilo lina uwezo wa kudumu kwa miaka 100 ijayo bila ya kupoteza
ubora wake na uhalisia kutokana na ujenzi wa kitaalam uliotumia vifaaa
vya kisasa na vyenye ubora zaidi.
Lekule
alisema usanifu wa jengo hilo ulianza Januari 2011 na ujenzi ulianza
Novemba 7, mwaka 2013 na sasa upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Naye
Meneja Uwekezaji wa NCAA, Needpeace Wambuge, alisema jengo hilo ni
maalum kwa ajili ya kitega uchumi cha biashara ya utalii ili kuendeleza
utalii baada ya kutokea kwa mtikisiko kwenye sekta hiyo, ulioathiri
shughuli za utalii sehemu mbalimbali nchini.
Aidha
alisema hadi sasa asilimia 45 ya jengo hilo limeshapangishwa na wadau
mbalimbali na gharama za ukusanyaji wa mapato kwa mwezi zitafikia kiasi
cha Sh. milioni 350, na kwa mwaka mzima kodi inayotarajiwa kukusanywa ni
Sh. bilioni 4.3.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni