Dstv Tanzania

MWENYEKITI WA BODI YA CHAI TANZANIA MHANDISI STEVEN MLOTE AMALIZA MGOGORO WA CHAI LUPEMBE NJOMBE


Na Elizabeth John, Njombe

Mwenyekiti wa Bodi ya Chai Tanzania Mhandisi  Steven Mlote  hatimaye amefanikiwa kuzikutanisha pande mbili zilizokuwa na mgogoro baina ya Muungano wa Vijiji vya Ushirika Lupembe (Muvyuu) dhidi ya Mwekezaji wa kiwanda cha Chai Igombola katika tarafa ya Lupembe mkoani Njombe.

Mgogoro huo uliodumu zaidi ya miaka nane tangu mwaka 2008 ulikuwa ukipelekea wakulima wa zao la chai katika Tarafa ya Lupembe kushindwa kufanya uzalishaji wa chai na kwenda kuuza katika kiwanda cha mwekezaji huyo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki na wakulima wa lupembe na mwekezaji, mhandisi Mlote amesema mgogoro huo umewaathiri kwa kiasi kikubwa wananchi wa Lupembe pamoja na taifa kwa sababu chai iliyokuwa inazalishwa Lupembe ilikuwa inashika nafasi ya kwanza kwenye soko la dunia.

“Tuanze uzalishaji mambo mengine yanayoendelea tuiachie serikali…Lupembe ilikuwa inazalisha chai bora ambayo ilikuwa na soko kubwa duniani, tangu mgogoro huu uanze kiwango cha uzalishaji kimeshuka,” amesema mhandisi Mlote.


Amesema kuwa ameapata taarifa kuna baadhi ya viongozi wananufaika na mgogoro huo hali iliyokuwa inapelekea kukosa suluhu na kwamba watu wote wanajulikana na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Majina ninayo ni viongozi wakubwa mmesababisha uchumi wa wana Lupembe kushuka wakati awali walikuwa ni wazalishaji wazuri wa chai mkoani Njombe,” amesema.

Aidha mhandisi Mlote pia amegusia suala la mali zilizokuwa za Muvyulu ambazo wazihujumu alisema  kwamba watapata tabu sana, wahusika wote wanajulikana.

“Wana Lupembe wameteseka kwa muda mrefu, kulikuwa na magari na mali nyingine nyingi, ambazo sizioni hata moja sijui mmepeleka wapi?” aliuliza mhandisi Mlote.


 Mwenyekiti huyo pia ameagiza iundwe bodi itakayosaidia kufuatilia kusiwepo tena na  mgogoro baina ya pande mbili hizo.


 Kwa upande wao baadhi ya wakulima wa chai akiwemo Daniel Makweta amesema kuwa kipato chao kinategemea uwepo wa kilimo cha chai, lakini wanakabuliwa na changamoto ya miundombinu inayopelekea kushindwa kusafirisha mazao ya chai kiwandani.

“Wamekubali mgogoro umeisha, lakini tunaomba viongozi wawe wawazi kwani sisi tunategemea kilimo cha chai, na mgogoro huu ulituathiri kwa kiasi kikubwa kwani tulikuwa tunalazimika kupeleka chai yetu mbali badala ya kiwanda ambacho tayari tuna hisa nacho,” amesema Makweta.


Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Muvyulu Andrea Ulungi amesema mbele ya Injinia Mlote kuwa wanaomba wasameheane katika kipindi chote cha mgogoro huo ili waweze kuendeleza kilimo cha chai kwa maslahi ya wakulima na mkoa kwa ujumla.


 Tukio la kuashiria mgogoro huo umemalizika baina ya pande hizo mbili lilihitimishwa kwa viongozi wa Muvyulu na mwekezaji wa kiwanda Yusuf Mullah kwa kushikana mikono mbele ya mwenyekiti huyo wa Bodi.


Mullah amesema kuwa wataendelea kushirikiana na pande zote na kwamba wanachohitaji ni kuendeleza uzalishaji wa kilimo cha chai katika Tarafa ya Lupembe.


“Tunafanya mgogoro siyo kwenye njaa ni kwenye neema hatujui, kwa upande wetu sisi tupo tayari kushirikiana kwa pande zote ili kwamba tulete haya maendeleo haraka sana, sasa tuchole mstari kwa sababu tunafanya mgogoro kwenye neema hata mwenyezi Mungu haelewi, nakuhakikisha hakutakuwa na mgogoro mwingine ila sisi kama wawekezaji hatukai hapa kila mmoja anavutia upande wake,” amesema Mullah.


 Mwisho.

Hakuna maoni: