Dstv Tanzania

SERIKALI YAJIPANGA KUNUNUA KOROSHO ZOTE

Rais Magufuli leo Novemba, 10, 2018 amekagua magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyoandaliwa kwa ajili ya kubeba korosho za wakulima endapo wanunuzi binafsi hawatatii maagizo ya Serikali ifikapo Jumatatu tarehe 12 Novemba, 2018 saa 10:00 Jioni.

“Nataka kuwahakikishia wakulima wa korosho Serikali ipo na itaendelea kuwapigania, ikifika Jumatatu saa 10:00 jioni, hawa wanunuzi binafsi hawajajitokeza na kueleza watanunua tani ngapi, Serikali itanunua korosho zote na fedha za kununulia zipo” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Rais Magufuli amefanya ukaguzi huo katika Kambi ya Jeshi ya Twalipo, Kikosi cha Usafirishaji cha 95KJ Mgulani Jijini Dar es Salaam ambapo magari 75 yenye uwezo wa kubeba tani 1,500 kwa mpigo yameandaliwa kwa ajili ya kubeba korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na Tanga.

Rais Magufuli amebainisha kuwa baada ya kununua korosho, Serikali itatafuta soko na korosho jingine zitakazobanguliwa kwaajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Rais Magufuli amesema Serikali inalazimika kuchukua hatua hizi baada ya wanunuzi binafsi kufanya mgomo wa kununua korosho kwa kusuasua licha ya kufanya nao mazungumzo na kufikia makubaliano tarehe 28 Oktoba, 2018 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Maafisa na Askari wa JWTZ waliokuwepo wakati wa ukaguzi huo, Rais Magufuli amesema, endapo wanunuzi binafsi hawatatii maagizo ya Serikali ya kununua korosho za wakulima kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kwa kilo, sambamba na kutii agizo lililotolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa, hakuna mnunuzi yeyote atakayeruhusiwa kununua korosho na Serikali itachukua hatua ya kutumia JWTZ na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kununua korosho zote za wakulima kwa bei ya zaidi ya shilingi 3,000 kwa kilo.

Hakuna maoni: